Mwanahabari wa Shirika la Utangazaji humu nchini KBC, Francis Ngala, ameshinda tuzo ya Podcast Bora ya Mwaka katika Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (AJEA) 2025 zilizoandaliwa na baraza la vyombo vya habari humu nchini MCK.
Ngala alitunukiwa tuzo hiyo katika hafla ya 13 ya AJEA iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Edge Convention Centre jijini Nairobi, ikimtambua kwa kazi yake ya kipekee ya podcast iliyopewa jina la “Jamii Inaweza Kutoa Mchango Gani Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi?”
Podcast hiyo ilichunguza namna mabingwa wa Weather Mtaani katika makazi duni ya Kibera wanavyowafikishia wakazi taarifa muhimu za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia lugha ya Sheng na mbinu nyingine zinazofahamika kwa urahisi na jamii.
Kazi hiyo iliangazia mchango wa jamii katika kuhamasisha uelewa wa masuala ya tabianchi na kuwajengea wananchi uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Tuzo hiyo inathibitisha nafasi ya KBC kama moja ya taasisi zinazoongoza katika matumizi ya mbinu bunifu za usimulizi wa habari na uandishi wa habari wenye athari chanya kwa jamii.
Akizungumza baada ya kutwaa tuzo hiyo, Ngala alieleza furaha yake na kutoa shukrani kwa KBC kwa kumpa fursa ya kukuza taaluma yake.
“Nina furaha sana kwa kupokea tuzo hii. Kwa kweli juhudi hulipa . Pia napenda kuishukuru KBC kwa kunipa fursa hii ya kuonyesha uwezo wangu na kuendelea kukua katika taaluma ya uandishi wa habari,” alisema.
Aliongeza kuwa ushindi huo unampa hamasa zaidi ya kuendelea kuandaa maudhui yenye manufaa kwa jamii, yanayolenga kuelimisha, kuhabarisha na kuhamasisha mabadiliko chanya.
Kufuatia ushindi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa KBC, Agnes Kalekye Nguna, alimpongeza Ngala kwa mafanikio hayo, akisema kuwa tuzo hiyo ni ushahidi wa kujituma, ubunifu na weledi wake katika kazi.
Katika ujumbe wake wa pongezi, Kalekye alisema mafanikio hayo si heshima kwa Ngala pekee bali pia ni fahari kwa shirika zima la KBC.
“Tuzo hii ni uthibitisho wa dhamira yako, ubunifu, taaluma na kujitolea kwako kwa viwango vya juu vya uandishi wa habari. Shirika linajivunia mafanikio yako kwani yanaonyesha nguvu ya juhudi zetu za pamoja na athari ya hadithi tunazosimulia kwa jamii,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa ushindi huo unaakisi dhamira ya KBC ya kuendelea kukuza uandishi wa habari bora unaolenga maslahi ya umma na kuibua mijadala yenye manufaa kwa jamii.
Tuzo za AJEA ni miongoni mwa tuzo zenye hadhi kubwa zaidi katika sekta ya habari nchini Kenya, zikilenga kutambua waandishi wa habari wanaoonyesha ubunifu, umahiri na weledi katika kazi zao.
Ushindi wa Ngala unaongeza orodha ya mafanikio ya KBC katika sekta ya habari na kuthibitisha nafasi ya shirika hilo kama kinara wa utangazaji wa umma na usimulizi wa hadithi zinazochochea maendeleo ya kijamii.