Maandalizi ya mvua ya El Nino yamepamba moto huku serikali ikiwataka Wakenya na asasi zingine husika kuchukua tahadhari za mapema.
Mvua hiyo inatarajiwa kuanzia mwezi Oktoba na kuendelea hadi mwezi Disemba mwaka huu, huku ikitarajiwa kuendelea hadi mapema mwaka 2027.
Kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa na Katibu wa Idara ya Utangazaji na Mawasiliano Stephen Isaboke na Msemaji wa serikali Charles Owino wamesema kuna haja ya kila mtu kukaa macho.
“Kama serikali, tunatoa wito kwa kila mmoja kujiandaa mapema. Hakuna hofu yoyote lakini kuna sababu ya taasisi za serikali, jamii na wananchi kuwa makini na kuchukua hatua mwafaka,” alisema Owino wakati akiwahutubia wanahabari leo Alhamisi.
Aidha, taarifa hiyo ilidokeza kuwa serikali imebuni mkakati unaoleta pamoja asasi mbalimbali kujiandaa kwa mvua hiyo, huku mashirika yote ya serikali yakitakiwa kubuni kamati za kitaifa za kukabiliana na majanga yatakayosababishwa na mvua hiyo.
Wakati huo huo, serikali za kaunti zimetakiwa kutambua maeneo yatakayoathiriwa na mvua hiyo, na kuanza maandalizi ya kuwahamishia wakazi maeneo salama.
“Wale wanaoishi karibu na kingo za mito, watahamishwa kabla ya kuanza kwa mvua hiyo,” aliongeza Owino.
Mara ya mwisho taifa hili kushuhudia mvua ya El nino ilikuwa mwaka 1997 huku mvua hiyo ikiendelea hadi mwaka 1998.