Muungano wa watayarishaji muziki nchini – Kenya Association of Music Producers (KAMP) – umemrejesha Angela Ndambuki kwenye wadhifa wa mwenyekiti.
Bi. Ndambuki alichaguliwa kwa muhula mwingine kama mwenyekiti wa muungano huo kwenye mkutano uliofanyika Juni 22, 2023.
Usimamizi wa muungano huo ulisema kwenye taarifa kwamba hatua hiyo ni ishara kwamba bodi inatambua uongozi mzuri wa Ndambuki pamoja na kujitolea kwake kazini na aliyofanikiwa kutimiza katika sekta ya muziki. Muungano wa KAMP unatambua Ndambuki kama nguzo muhimu katika kupigania haki za watayarishaji muziki na wanamuziki nchini Kenya.
Wakati wa kipindi chake cha kwanza cha uongozi, Bi. Angela Ndambuki alihakikisha kutolewa upya kwa leseni ya muungano huo na bodi ya hakimiliki nchini Kenya almaarufu “Kenya Copyright Board (KECOBO)” baada ya miaka miwili.
Alihakikisha pia kwamba mirahaba ya watayarishaji muziki imeongezeka na akaongoza ziara ya kwanza ya kujifahamisha hadi nchini Afrika Kusini ambapo walitia saini maelewano na muungano sawia nchini humo almaarufu South African Music Performance Rights Association (SAMPRA).
Ndambuki anahudumu pia kama mkurugenzi wa shirikisho la tasnia ya muziki yaani “International Federation of the Phonographic Industry (IFPI)” katika eneo la Sub-Saharan Africa.