Afueni kwa Oduol baada ya Seneti kupinga kutimuliwa kwake

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Gavana wa kaunti ya Siaya William Oduol amekwepa shoka la kutimuliwa kwenye wadhifa wake.

Hii ni baada ya Maseneta kupiga kura kupinga ripoti ya kamati maalum iliyokuwa imependekeza kutimuliwa kwake.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Seneta William Kisang ilikuwa imependekeza kutimuliwa kwa Oduol ikisema mashtaka mawili ya ukiukaji wa katiba na utumiaji mbaya wa mamlaka yalithibitishwa.

Katika shtaka la kwanza, Maseneta 27 walipiga kura kupinga shtaka hilo huku 16 wakiliunga mkono katika zoezi lililoegemea mirengo hasimu ya kisiasa nchini.

Katika shtaka la pili la utumiaji mbaya wa wadhifa wake, wembe ulikuwa huohuo baada ya Maseneta 27 kwa mara nyingine kupiga kura kupinga shtaka hilo huku 16 wakiliunga mkono.

Hususan, kura hiyo ilidhihirisha kuwa utawala wa Kenya Kwanza una usemi mkubwa katika mabunge yote kuliko mrengo wa upinzani wa Azimio.

“Wembe ulioshuhudiwa katika bunge la Kitaifa wakati wa upigaji kura wa Mswada wa Fedha 2013 ndio mtakaoshuhudia papa hapa katika bunge la Seneti,” alionya Seneta wa Nandi Samson Cherargei hata kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza.

Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi alisema kupingwa kwa mashtaka hayo mawili katika ukumbi wa Seneti kunamaanisha kuwa Oduol ataendelea kuhudumu katika wadhifa wake.

Aidha hatua hiyo inamaanisha kuwa ameponea kwa tundu la sindano kuwa Naibu Gavana wa kwanza kuwahi kutimuliwa tangu kuasisiwa kwa ugatuzi.

Wawakilishi Wadi wote 42 wa bunge la kaunti ya Siaya waliazimia kumtimua Oduol kufuatia mapendekezo ya jopo la wanachamana 14 lililobuniwa kumchunguza.

Katika kuchukua hatua hiyo, walimtuhumu, kwa miongoni mwa mambo mengine, kukiuka katiba na kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo.

Oduol alikanusha mashtaka yote dhidi yake.

Uhusiano mzuri ulioshamiri kati ya Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo na mgombea mwenza wake wakati huo William Oduol ulizorota kuanzia mwishoni mwa mwaka uliopita huku Oduol akimnyoshea Orengo kidole cha lawama kwa kukimya wakati kukiwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *