Wizara ya uchukuzi inasema imepiga hatua za kuhakikisha usalama barabarani, ili kukabiliana na ajali hizo zinazokithiri kote nchini.
Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema maagizo yaliyotolewa mapema mwezi Aprili yakitekelezwa kikamilifu yataokoa maisha ya watu wengi.
Kulingana na wizara hiyo, taasisi na kampuni zote zilipewa muda wa wiki mbili kuwasilisha magari kwa ukaguzi haswa wa kwa vidhibiti mwendo.
Magari ya kubebea abiria na ya kibiashara vile vile yalihitajika kufanyiwa ukaguzi au kupokonywa leseni na mamlaka ya uchukuzi nchini- NTSA.
Murkomen ameongeza kuwa wizara yake kwa ushirikiano na polisi wa Kitaifa na NTSA watahakikisha kuwa Sheria zote zinazingatiwa ,ili kuhakikisha usalama barabarani.
Hata hivyo, waziri huyo amesema kando na utekelezaji wa hatua hizo, wizara yake pia inawataka madereva kuchukua tahadhari na kujali usalama wao binafsi na wa abiria, ili kutekeleza jukumu lao katika kupunguza ajali za barabarani.