Mudavadi azindua mpango wa mazingira Uasin Gishu

Alielezea kwamba ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa Kenya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi jana aliongoza uzinduzi wa mpango jumuishi wa usimamizi wa rasilimali asilia wa thamani ya shilingi bilioni 34.

Alielezea kwamba ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa Kenya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa chakula.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika Kaunti ya Uasin Gishu, Mudavadi alisema mabadiliko ya tabianchi tayari yanaathiri kilimo, rasilimali za maji na maisha ya wananchi, hivyo kuifanya kuwa muhimu kwa serikali kutekeleza suluhisho za vitendo na za muda mrefu.

Mpango huo, unaofadhiliwa na Serikali kwa ushirikiano na Hazina ya Kimataifa ya Maendeleo ya Kilimo, IFAD, unatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu milioni mbili kutoka zaidi ya familia 407,000 zilizo katika mazingira hatarishi katika kaunti 10.

Kaunti zitakazonufaika ni Elgeyo Marakwet, West Pokot, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Nandi, Kakamega, Kericho, Kisumu, Homa Bay na Migori.

Mudavadi alisema mpango huo utaimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kurejesha mifumo ikolojia iliyoharibika, kuboresha uhifadhi wa maji na kuimarisha usalama wa chakula katika kaunti zinazoshiriki.

Alibainisha kuwa wakulima watapatiwa mbinu endelevu za usimamizi wa ardhi zitakazoongeza uzalishaji wa kilimo huku zikihifadhi rasilimali za asili.

Kwa mujibu wa Mudavadi, uwekezaji huo pia unatarajiwa kuongeza kipato cha familia, kuunda nafasi za ajira na kuimarisha ustahimilivu wa jamii za vijijini.

Share This Article