Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania Paul Makonda amesema kwamba anatizamia ujenzi wa msikiti mkubwa jijini Arusha.
Makonda ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini,alisema kwamba mbali na kuwa sehemu ya ibada, msikiti huo mkubwa utakuwa pia kivutio cha utalii.
Kiongozi huyo amesema pia kwamba Arusha inapaswa kutumia fursa zinazotokana na wageni na matukio makubwa yanayofanyika Jijini humo ili kuongeza shughuli za biashara na kukuza uchumi wa wananchi.
“Tuna mpango mkubwa hapa Arusha wa kujenga msikiti, sio wa Watu kuishia kuswali tu, bali utalii; yaani mtu akifika anaenda kutalii,” amesema Makonda.
Aidha, Makonda amepongeza viongozi walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa uongozi ni dhamana na jukumu la kusukuma mbele maono ya Taifa.
Makonda aliyasema hayo katika hafla ya uapisho wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nicodemus Mwikozi.