Harmonize kufuatiliwa kwa mwezi mmoja na BASATA

Tayari ametimiza masharti aliyokuwa amewekewa na BASATA na kuruhusiwa kuendelea na kazi zake.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii wa muziki nchini Tanzania Harmonize atakuwa chini ya uangalizi wa Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA, hata baada ya kutimiza masharti aliyowekewa awali.

Katika taarifa, Baraza hilo limesema Harmonize alifika BASATA Oktoba 2, 2026 na kutekeleza masharti hayo, lakini ataendelea kuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha mwezi mmoja.

BASATA imeonya kuwa haitasita kuchukua hatua dhidi ya Harmonize endapo hatatekeleza masharti aliyowekewa katika kipindi hicho.

Aidha, Baraza hilo limewataka Wasanii kuendelea kuzingatia Sheria, Kanuni, miongozo na maadili yanayosimamia shughuli za sanaa Nchini Tanzania, ikiwemo katika uzalishaji na usambazaji wa kazi za sanaa.

Harmonize alijipata matatani kutokana na wimbo wake uitwao, “Kudos” ambao unasemekana kutokidhi mahitaji ya maadili ya Tanzania.

Katika kumwadhibu msanii huyo BASATA ilimwagiza aondoe video ya wimbo huo kwenye majukwaa yote ya mitandao nchini Tanzania na alipe faini ya shilingi milioni 5 pesa za Tanzania katika muda wa siku 14 na asijihusishe na shughuli za sanaa kabla ya kutimiza hilo.

Mwelekezi wa video hiyo, Kennedy Sanga, naye alichukuliwa hatua zinazofanana.

BASATA ni shirika la serikali ya Tanzania lililojukumiwa kusimamia, kuratibu na kukuza maendeleo ya sekta ya sanaa, muziki na sanaa za maonyesho nchini Tanzania.

Share This Article