Maafisa kutoka asasi mbali mbali za usalama wamewapata mbuzi 167 waliokuwa wameibwa katika kaunti ya Isiolo.
Opresheni hiyo ilitekelezwa baada ya maafisa hao kupokea ripoti kuhusu wizi huo. Walichukua hatua za haraka na kuwaandama majangili hao na kuwafumania.
Kupitia kwenye ukurasa wa X, Huduma ya Taifa ya Polisi ilisema majambazi hao walitoroka baada ya kuwaona maafisa hao wa usalama, na kuwaacha nyuma mifugo hao.
“Mifugo hao waliokolewa na kurejeshwa kwa wamiliki wao halali,” ilisema Huduma ya Taifa ya Polisi.
Aidha, huduma hiyo iliwapongeza maafisa hao wa vitengo mbali mbali kwa kuchukua hatua za haraka, wakati huhuo ikiwapongeza wananchi kwa kutoa habari kwa wakati zilizofanikisha operesheni hiyo.