Mmoja wa matapeli aliyekuwa akisakwa kwa madai ya kuhusika katika udanganyifu wa mtihani wa KCSE mwaka huu, Collins Kipchumba Kemboi ametiwa mbaroni katika eneo la Kiamunyi mjini Nakuru.
Huku akijisingizia kuwa mwanamke kwa jina Dorothy Jerop Kiprono, mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 23, alikuwa amebuni kundi la watu zaidi ya 78,000 waliotaka kushirikishwa kwenye udanganyifu huo kwenye mtandao wake wa Telegram na wengine zaidi ya 8,500 katika vikundi vyake vya WhatsApp.
Kufuatia msako mkali uliotekelezwa na maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai DCI, kwa ushirikiano na wale wa Baraza la Kitaifa la Mitihani na maafisa wa serikali ya Kaunti ya Nakuru, mshukiwa huyo alikamatwa nyumbani kaunti ya Nakuru.
Kulingana na DCI, mshukiwa huyo alikamatwa na vifaa kadhaa vya kielektroniki, vikiwemo; simu ya rununu aina ya Infinix Hot 10 Lite, kadi kadhaa za simu, vitambulisho vya taifa vikiwa na majina tofauti na leseni ya kuendesha gari.
Mshukiwa huyo, ambaye amehitimu kwa Shahada ya Sanaa katika Usimamizi wa wafanyikazi ni mwajiriwa wa kampuni moja ya kimataifa.
Idara ya Upelelezi imesema atasalia rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nakuru, akisubiri kufikishwa Mahakamani.