Mahakama imeamuru kuwa mwanamume aliyedaiwa kusaidia katika utupaji wa mwili wa Willis Ayieko ambaye hadi kuuawa kwake alikuwa Meneja wa Idara ya Wafanyakazi wa kampuni ya Wells Fargo azuiliwe kwa siku 21.
Agizo hilo limetolewa na Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama ya Siaya Benjamin Limo.
Samwel Onyango, mwenye umri wa miaka 52, alifikishwa mahakamani leo Jumatano.
Hii ni baada ya mshukiwa huyo kukamatwa katika eneo la Luanda Doho huko Kisa Magharibi, kaunti ya Kakamega jana Jumanne.
Onyango alikamatwa na maafisa wa polisi wanaochunguza mauaji hayo.
Alipofikishwa mahakamani leo Jumatano, hakukiri mashtaka kwani polisi waliwasilisha ombi la kutaka azuiliwe kwa siku 21 ili kuwasaidia katika uchunguzi.
Mahakama iliridhia ombi hilo.
Mshukiwa anadaiwa kusaidia katika usafirishaji wa mwili wa Ayieko uliopatikana ukiwa umetupwa kwenye mto Mungowere ambao ni mpaka kati ya kaunti za Siaya na Kakamega Oktoba 23, 2024.
Onyango anakuwa mshukiwa wa tano kuamriwa kuzuiliwa na polisi ili kusaidia katika uchunguzi wa mauaji hayo.
Washukiwa wengine wawili, mwanamume na mwanamke, wamefariki baada ya kufyatuliana risasi na maafisa wa polisi wanaochunguza mauaji hayo.
Marehemu Ayieko alizikwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika kijiji cha Ong’iende katikati mwa kata ya Alego, kaunti ya Siaya.