Maafisa wa upelelezi wa Mombasa Mjini hatimaye wamemkamata Abdallah Suleiman, anayejulikana pia kama Asuu, mshukiwa mashuhuri wa kuwekea watu dawa kwenye vinywaji, ambaye amekuwa akisakwa kwa muda sasa.
Maafisa hao walikuwa wakimfuatilia baada ya kesi kadhaa za kutumia dawa za kulevya na wizi kuripotiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Mombasa.
Asuu ndiye alikuwa kinara wa kuhadaa abiria wasio na hatia wanaosafiri kuelekea Mombasa, Kisumu, Tanzania na maeneo mengine, kisha kuwaibia pesa na mali zao baada ya kuwapa dawa za usingizi.
Hata hivyo hakuwa na bahati aliponaswa katika Daraja la Mizani la Mariakani, ambapo maafisa wa upelelezi waliokuwa macho walipanda basi lililokuwa linaelekea Nairobi na kukomesha msururu wake wa uporaji kwa kutumia dawa.
Kwenye begi lake la ujanja, maafisa walikuta vidonge vya Lorivan 2, vinywaji baridi na vitafunio vinavyoshukiwa kuwa na dawa za kulevya, vyote vikiwa tayari kwa wahanga wake wengine wasiojua.
Kwa sasa, Asuu yuko korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani huku uchunguzi ukiendelea.