Mlimbwende mahakamani kwa kukiuka sheria za trafiki Rwanda

Marion Bosire
2 Min Read

Divine Muheto ambaye alishinda taji ya ulimbwende nchini Rwanda mwaka 2022 alifikishwa katika mahakama ya Kicukiro leo Alhamisi Oktoba 31, 2024 kufuatia makosa ya trafiki.

Upande wa mashtaka unataka Muheto ahukumiwe kifungo cha miezi 20 gerezani, 12 kwa kosa la kutoroka eneo la tukio, 8 ya kuendesha gari bila lesena na 6 kwa kosa la kuendesha gari akiwa mlevi.

Kiongozi wa mashtaka alielezea mahakama kwamba Oktoba 24, 2024, Muheto aligonga mlingoti wa stima na mti aina ya mtende kabla ya kukwepa.

Alipopimwa baada ya kukamatwa, ilibaikika kwamba kiwango cha pombe kwenye mwili wake kilikuwa cha juu kuliko kinachoruhusiwa.

Muheto alikamatwa na maafisa wa polisi Jumanne Oktoba 29, 2024 baada ya kutekeleza makosa ya kuendesha gari akiwa mlevi na kuendesha gari bila leseni.

Polisi wanasema aliharibu miundombinu alipokuwa akiendesha gari katika hali hiyo na kwamba alitoroka kutoka eneo la tukio na kwamba sio mara ya kwanza anatekeleza makosa hayo.

Divine alijulikana ndani na nje ya Rwanda mwaka 2022 baada ya kuibuka mshindi wa shindano la Miss Rwanda, shindano lililokomeshwa na serikali baada ya waandalizi kutuhumiwa kwa utovu wa maadili.

Rwanda ina sheria kali za trafiki na adhabu ya kosa la kuendesha gari ukiwa mlevi ni faranga elfu 150, sawa na shilingi elfu 14 200 za Kenya.

Mkosaji anaweza pia kuwekwa rumande kwa muda wa siku tano kabla ya kufikishwa mahakamani.

Share This Article