Mkuu wa vikosi vya ulinzi KDF, Francis Ogolla na Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome, walizuru eneo la Tiaty kaunti ya Baringo kukadiria hali ya usalama .
Ziara ya wawili hao siku ya Alhamisi, inajiri huku visa vya utovu wa usalama vikiendelea kuripotiwa katika eneo hilo.
Walipozuru kituo cha polisi cha Kolowa, Inspekta huyo mkuu wa polisi, aliwapongeza maafisa wa polisi katika juhudi zao za kukabiliana na ujangili katika eneo la bonde la Kerio.
Huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa jukumu linalotekelezwa na asasi mbali mbali za usalama, Koome alisifu ushirikiano wa huduma ya polisi na vikosi vya ulinzi katika kuboresha hali ya usalama katika Kaunti ya Baringo.
Wakuu hao wawili wa usalama pia walitangamana na jamii, ili kufahamu maswala ya usalama yanayowakumba.
Baadaye walizuru shule ya msingi ya Kolowa kukadiria shughuli za ukarabati zinazoendelea.