Mikie Wine amtetea Bobi Wine kwa kutohudhuria tamasha lake

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Michael Mukwaya maarufu kama Mikie Wine amemtetea kakake mkubwa Bobi Wine kwa kutohudhuria tamasha lake wikendi iliyopita.

Mikie aliandaa tamasha katika eneo la Jahazi Pier huko Munyonyo, onyesho ambalo kulingana na wadadisi lilifanikiwa.

Akizungumza na wanahabari, Mikie alisema kwamba kakake hangeweza kuhudhuria tamasha hilo kwani bado anauguza jeraha la mguu baada ya kugongwa na kopo la gesi ya kutoza machozi kwenye mvutano na maafisa wa polisi.

“Lilikuwa tamasha la Mikie Wine, naamini waliohudhuria walikuja kuniona na kunisikiliza.” alisema Mikie akiongeza kwamba Bobi ambaye pia ni mwanasiasa, kiongozi wa upinzani huwa na shughuli nyingi.

Mikie Wine, Gravity Omutujju na Qing Madi ambao wote ni wanamuziki nchini Uganda, waliandaa matamasha wikendi iliyopita huku ya Mikie na Gravity yakikiwa siku ya Jumamosi.

Tamasha la Mikie liliandaliwa katika eneo la Jahazi Pier huku Gravity akiandaa lake kwenye uwanja wa Lugogo ambao hauko mbali sana na Jahazi.

Gravity alitangulia kutangaza tamasha lake na wadadisi wa tasnia ya burudani nchini humo wanahisi wawili hao walikuwa wanapimana nguvu ikitizamiwa kwamba uhusiano kati ya Gravity na kakake Mikie sio mzuri kama awali.

Share This Article