Mikahawa mingi mjini Naivasha na viunga vyake imeongeza bei maradufu huku mashabiki wakifurika mjini Naivasha kushuhudia makala ya mwaka 2023 ya WRC Safari Rally ambayo yameanzishwa rasmi Alhamisi adhuhuri katika bustani ya Uhuru, kaunti ya Nairobi.
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na KBC Digital, baadhi hoteli zilizokuwa zikitoza shilingi 1,500 kwa usiku zinatoza shilingi 2,500 huku baadhi ya waliokuwa wakitoza shilingi 2,000 wakiongeza hadi shilingi 4,000 kwa usiku mmoja.
Vyumba maarufu kama Airbnb ambavyo vimekuwa vikitoza shilingi 6,000 vimeongezwa bei hadi shilingi 10,000 kwa siku.
Baadhi ya wamiliki na wahudumu wa mikahawa wanakisia kuongeza bei zaidi ya maradufu ifikiapo Ijumaa wakati magari yatakuwa yakishindana mjini Naivasha na viunga vyake kwa umbali wa takriban kilomita 350.