Mahakama ya Kwale imeridhia kuzuiliwa kwa raia wa Uholanzi Elwin Ter Horst kwa siku 14 kwa kushukiwa kumdhulumu afisa wa polisi wa kituo cha Diani.
Hakimu Mkuu wa Mahakama hiyo Joy Mutimba aliitikia ombi la kiongozi wa mashtaka aliyetaka muda zaidi wa kufanya uchunguzi kwa madai mengine ya kesi hiyo, kama vile uharibifu wa mali, dhuluma, kukataa kukamatwa, kuleta usumbufu na ulanguzi wa mihadarati.
Naibu Kiongozi wa Mkurugenzi wa Mashtaka Rosemary Nandi aliiambia mahakama kuwa wachunguzi walihitaji muda kufanya uchunguzi wa kina kwa kesi hiyo, ikiwemo kamera za CCTV.
Ter Horst, mwenye umri wa miaka 47, alikamatwa Oktoba 28 katika eneo la Boma Banda huko Diani akimdhulumu mpenzi wake raia wa Kenya na baadaye kuripotiwa kumshambulia polisi.