Waziri wa Leba Dkt. Alfred Mutua amebuni kamati inayoleta pamoja wizara mbalimbali ili kuongoza mazungumzo kati ya serikali na wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu wanaogoma.
Dkt. Mutua alitangaza kubuniwa kwa kamati hiyo baada ya kukutana na viongozi wa Chama cha Wahadhiri (UASU) na kile cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) katika jengo la NSSF leo Jumatano asubuhi.
Waziri alisema kamati hiyo itakutana kesho Alhamisi kujadiliana juu ya mbinu ya kusitisha mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi hao unaoendelea na kuhakikisha wanarejea kazini.
“Mazungumzo ya hapo kesho yataiwezesha serikali kufikia makubaliano na UASU na KUSU na kimsingi kusitisha mgomo unaoendelea,” Dkt. Mutua alielezea imani wakati wa mkutano huo.
Wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu wanashinikiza kutekelezwa kikamilifu kwa Mkataba wa Maelewano (CBA) wa mwaka 2021-2025 ambao ikiwa utatekelezwa, utakuwa chanzo cha wao kupata nyongeza ya mshahara na bima bora ya afya miongoni mwa manufaa mengine.