Mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu wamalizika

Martin Mwanje
3 Min Read

Wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakigoma kwa kipindi cha wiki moja iliyopita wametangaza kumalizika kwa mgomo wao. 

Hii ni baada ya wao, kupitia Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu UASU na kile cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) kufikia makubaliano na serikali wakati wa mkutano uliofanyika leo Alhamisi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Leba Dkt. Alfred Mutua na Katibu wa Idara ya Elimu ya Juu Dkt. Beatrice Inyangala.

“Nataka kuiambia nchi yote kuwa kwamba tumefikia makubaliano. Tumechukua matunda yanayoning’inia, masuala yaliyosalia yatakamilishwa katika kipindi cha mwezi mmoja ujao,” alisema Dkt. Constantine Wesonga, Katibu Mkuu wa UASU.

“Tunakusanyika kusema kuwa tumefikia makubaliano. Tumekuwa tukigoma na tumegoma hadi tumefikia makubaliano,” aliongeza Dkt. Charles Mukhwaya, Katibu Mkuu wa KUSU.

“Punde baada ya kutekelezwa kwa makubaliano haya, mgomo utakuwa umemalizika.”

Dkt. Inyangala akizungumzia makubaliano yaliyoafikiwa alielezea furaha yake kufuatia kusitishwa kwa mgomo huo akisema masomo sasa yataerejelewa kama kawaida katika vyuo vikuu.

Alielezea kujitolea kwa serikali kuangazia maslahi ya wafanyakazi wa vyuo vikuu nchini.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, hakuna mfanyakazi aliyegoma atadhulumiwa na kwamba na kwamba wahadhiri watalipwa mara moja mshahara wa kila mwezi kwa mujibu wa viwango vilivyokubaliwa na kamati kati ya wizara.

Makubaliano hayo yanaelezea kuwa wahadhiri walio katika makundi ya 13A, 14A NA 15A watalipwa mshahara kwa kiwango cha asilimia 7 wakati wale walio katika makundi ya 10A, 11A na 12A wakilipwa mshahara wa kila mwezi kwa asilimia 10.

Wafanyakazi wa vyuo vikuu walio katika makundi ya 13, 14 na 15 pia watalipwa mshahara wa kila mwezi kwa kiwango cha asilimia 7 wakati wale walio katika makundi ya 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11 na 12 wakilipwa kwa kiwango cha asilimia 10.

Pande zote husika zimepangiwa kukutana tena kufikia kesho Ijumaa kuanzisha mazungumzo ya viwango vya mshahara vya mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/2025.

Viwango hivyo vipya vitalipwa katika mishahara ya mwezi Oktoba mwaka huu.

Jana Jumatano, Waziri wa Leba Dkt. Alfred Mutua alibuni kamati kati ya wizara ili kuongoza mazungumzo kati ya serikali na wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu waliogoma.

Dkt. Mutua alitangaza kubuniwa kwa kamati hiyo baada ya kukutana na viongozi wa UASU na KUSU katika jengo la NSSF.

Waziri alielezea matumaini kuwa kamati hiyo itasaidia pande zote mbili kufikia makubaliano, matumaini ambayo leo yametimia.

“Mazungumzo ya hapo kesho (leo Alhamisi) yataiwezesha serikali kufikia makubaliano na UASU na KUSU na kimsingi kusitisha mgomo unaoendelea,” Dkt. Mutua alielezea imani wakati wa mkutano huo.

Wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu walikuwa wakishinikiza kutekelezwa kikamilifu kwa Mkataba wa Maelewano (CBA) wa mwaka 2021-2025 ambao ikiwa utatekelezwa, utakuwa chanzo cha wao kupata nyongeza ya mshahara na bima bora ya afya miongoni mwa manufaa mengine.

Share This Article