Mfalme wa Uingereza Charles III na mkewe Malkia Camilla watafanya ziara ya kiserikali ya siku nne nchini Kenya kuanzia mwisho wa mwezi huu, Kasri la Buckingham lilitangaza Jumatano.
“Mfalme na Malkia watafanya ziara ya siserikali nchini Kenya, kuanzia Jumanne, tarehe 31 Oktoba hadi Ijumaa, Novemba 3, 2023, kusherehekea uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili na ushirikiano thabiti na wenye nguvu wanaoendelea kuuanzisha,” ilisema ikulu.
Ziara hiyo inajiri huku Kenya ikijiandaa kusherehekea miaka 60 ya uhuru.
Itakuwa ziara ya kwanza ya Mfalme Charlse katika taifa la Jumuiya ya Madola ikizingatiwa kwamba ni nchi ambayo utawala wa Malkia Elizabeth II ulianza, baada ya kuchukua kiti cha enzi nchini Kenya mnamo Februari, 1952.
Mfalme na Malkia wanatarajiwa kuzuru kaunti za Nairobi na Mombasa na maeneo jirani.
”Mpango wa Mfalme utaakisi njia ambazo Kenya na Uingereza zinafanya kazi pamoja, hasa ili kuimarisha ustawi wa pande zote, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kukuza fursa na ajira kwa vijana, kuendeleza maendeleo endelevu na kuunda eneo lenye utulivu na usalama zaidi,” ilisema taarifa rasmi iliyotolewa na tovuti ya serikali ya Uingereza.