Mwanasiasa Rose Mbithe Mulwa almaarufu Rose Mbithe Ndetei na wanawe Chris Mulwa na Agnes Mulwa sasa watazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kileleshwa wakisubiri kufikishwa mahakamani keshokutwa Alhamisi.
Watatu hao watafikishwa mbele ya Jaji Kanyi Kimondo wakikabiliwa na mashtaka ya kupanga na kufadhili mauaji ya Dkt. Victoria Nthunya Mutiso.
Dkt. Mutiso aliuawa na watu wasiojulikana katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi Julai 29 mwaka huu.
Uchunguzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI ulibaini kuwa washukiwa hao watatu walikula njama na maafisa wa polisi kumuua Dkt. Mutiso mwishoni mwa mwezi jana.
DCI ikimtambua Konstebo Elijah Kibelion Kimoi kama afisa aliyefyatua risasi na kumuua Dkt. Mutiso kwenye tukio hilo lililotokea majira ya asubuhi.
Idara hiyo inayoongozw ana Mohamed Amin iliashiria kuwa ilikuwa ikimtafuta afisa mwingine, Inspekta Kenneth Kipkong Kipkemboi anayesimamia kituo cha polisi cha Nderi kwa madai ya kuratibu fedha na kutoa silaha iliyotumiwa katika mauaji hayo.
Uchunguzi umebaini kuwa kiini cha mauaji hayo ni mzozo wa ardhi iliyopo katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos.
DCI inaamini kuwa ni mzozo huo ambao yamkini ulisababisha kifo cha wakili Kyalo Mbobu mwezi Septemba mwaka jana.
Taarifa hii imechangiwa na mwanahabari wetu Ruth Wambui.