21 wafika fainali shindano la Miss Universe Tanzania 2026

Fainali inatarajiwa kufanyika Septemba 5, 2026, katika ukumbi wa Superdome Masaki, Dar es Salaam.

Marion Bosire
2 Min Read

Kina dada 21 wameingia hatua ya fainali ya mashindano ya ulimbwende ya Miss Universe Tanzania 2026, baada ya kufanyika kwa hafla ya kuwavisha mikanda yaani ‘Sashing Ceremony’ ambapo washiriki hao walikutana.

Fainali ya Miss Universe Tanzania 2026 inatarajiwa kufanyika Septemba 5, 2026, katika ukumbi wa Superdome Masaki, Dar es Salaam, ambapo mshindi atapatikana baada ya mchuano wa washiriki hao.

Awali, mashindano hayo yalipangwa kuwa na washiriki 20 wa fainali, lakini Mkurugenzi wa Miss Universe Tanzania, Millen Magese, akaongeza mshiriki mmoja, Mariam Khatib.

Bi Khatib ni mlemavu wa ngozi yaani zeruzeru na amekuwa akionyesha maendeleo mazuri zaidi wakiwa kambini.

Hatua hiyo imefanya idadi ya wanafainali kufikia 21, ambao sasa wanaendelea na maandalizi ya kuwania taji la Miss Universe Tanzania 2026.

Warembo hao wanajumuisha Makini Nzunda wa mkoa wa Rukwa, Melinda Enock mwakilishi wa mkoa wa Kagera, Beatrice Romward anayewakilisha Mtwara, Diana Ibrahim mwakilishi wa Mbeya, Irene Mbando na Mariam Khatib wa Pwani.

Wengine ni Rachel Osward Shonza wa mkoani Songwe, Saraphina Blassius mwakilishi wa mkoa wa Mara, Sandra Giovinazzo mwakilishi wa Arusha, Queen Elizabeth Makune wa Mwanza, Saraphina Kiyosaki wa Manyara, Diana Swai wa Zanzibar, Merikai Wavii wa Arusha, Cyler Henry kutoka Kilimanjaro na Mariam Cosmas wa mkoa wa Simiyu.

Maria Masuke wa Kigoma, Inviolata Frank wa Dar es Salaam, Ignacia Emmanuel wa Singida, Farida Kanda wa Morogoro, Catherine Kayanda wa Dodoma na Magdalena Daudi mwakilishi wa mkoa wa Geita wanakamilisha orodha hiyo.

Share This Article