Wizara ya Fedha imewaagiza maafisa wakuu wa uhasibu katika mashirika ya serikali na asasi huru, kuangazia zaidi malipo ya madeni kabla ya kukamilika kwa kipindi cha fedha cha mwaka huu.
Data kutoka wizara hiyo zinaonyesha kuwa kati ya shilingi bilioni 537.2 ambazo serikali inadaiwa na wafanyabiashara na wanakandarasi, mashirika ya serikali yanawajibikia shilingi bilioni 450.2 za deni hilo.
Kupitia ilani iliyotumwa kwa maafisa wakuu wa mashirika na asasi huru za serikali, manaibu chansela wa vyuo vikuu vya umma, pamoja na wakuu wa taasisi za kutoa mafunzo ya kiufundi na zile za kutoa mafunzo kwa walimu, Waziri wa fedha na Mipango ya Kitaifa Profesa Njuguna Ndung’u aliwaagiza maafisa hao kutekeleza maagizo hayo ambayo hayajumuishi utoaji wa kandarasi mpya.
Katika bajeti ya ziada, serikali imetenga shilingi bilioni 60 kutumika kulipia madeni hayo.
Mchakato huo unatarajiwa kuboresha shughuli za kiuchumi, hususan miongoni mwa biashara ndogo ndogo ambazo uwezo wao wa kifedha ulikuwa umeathirika pakubwa.
Wizara ya Fedha inapanga kubuni kamati ya kutathmini madeni yanayodaiwa mashirika ya serikali kwenye kipindi kijacho cha fedha ili kusaidia kuhakiki madeni hayo na kutoa ushauri jinsi yatakavyolipwa.
“Punde tu madeni yatakapolipwa, hazika kuu itaagiza wahusika wote kutekeleza kikamilifu sheria kuhusu usimamizi wa fedha ya mwaka 2012,” alisema Profesa Ndung’u.