Uvunaji mahindi waanza kwenye mradi wa Galana Kulalu

Tom Mathinji
2 Min Read
Uvunaji mahindi waanza katika shamba la Galana Kulalu.

Awamu ya kwanza ya uvunaji mahindi katika mpango wa unyunyizaji maji mashamba wa Galana Kulalu, ulianza leo Jumamosi.

Mradi huo unaolenga kuhakikisha utoshelevu wa chakula hapa nchini, unatekelezwa chini ya mpango wa ushirikiano kati ya sekta ya kibinafsi na serikali, kwenye shamba la serikali katika kaunti za Kilifi na Tana River.

Akizungumza aliposhuhudia uvunaji huo, Waziri wa Maji na Unyunyizaji Mashamba Maji Eric Mugaa, alisema mradi huo utapunguza gharama ya uagizaji chakula kutoka nje kwa shilingi bilioni 500.

“Mradi wa Galana Kulalu,unapiga jeki mfumo wa kuimarisha uchumi kutoka chini wa Bottom Up. Tumejitolea kuhakikisha mradi huo unafanikiwa,” alisema Mugaa.

Kulingana na waziri huyo, mahindi kwenye ekari 330 kati ya 1,500 itavunwa katika muda wa siku tano zijazo.

Aliongeza kuwa mpango wa muda mrefu wa ujenzi wa bwawa kubwa la maji unatekelezwa ili kunyunyiza maji kwa ekari 200,000.

Kwa upande wake, katibu katika idara ya unyunyizaji mashamba maji Ephantus Kimotho, aliyekuwa ameandamana na waziri Mugaa, alisema ni bayana kwamba kupitia unyunyizaji mashamba maji, sehemu kame hapa nchini zinaweza zalisha chakula na kuhakikisha utoshelevu wa chakula hapa nchini.

Katibu huyo alidokeza kuwa, serikali inashirikiana na washirika wengine kunyunyiza maji ekari 180,000 ya mashamba.

Uvunaji huo wa kwanza wa katika mradi wa uzalishaji chakula wa Galana Kulalu, unaashiria mwanzo wa safari ya uzalishaji endelevu wa mbegu za ubora wa hali ya juu, na kutimiza kujitolea kwa serikali kutekeleza mfumo wa kisasa katika sekta ya kilimo.

Website |  + posts
Share This Article