Wakazi wa Nyandarua wahimizwa kukataa siasa za migawanyiko

Lydia Mwangi
2 Min Read
Wakazi wa Nyandarua wahimizwa kupiga kumbo siasa za migawanyiko.

Wakazi wa Kaunti ya Nyandarua wametakiwa kujivunia utajiri wa rasilimali walizonazo, na kuepuka siasa za migawanyiko, huku wakihimizwa kuchangamkia nafasi zilizotolewa kupitia Mpango wa NYOTA unaolenga vijana kote nchini.

Waziri wa Utalii Rebecca Miano na Katibu katika wizara ya Uchukuzi Mhandisi Joseph Mbugua, walitoa wito huo walipohutubia wakazi katika Shule ya Msingi ya Mwiteithie, eneo la Kinangop.

Waziri Miano alisema Kenya inalenga kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka wa 2032, ambapo tayari miti bilioni 1.5 imepandwa.

Alimpongeza Rais William Ruto kwa kuongoza mpango huo kwa mfano, akisisitiza kuwa ni jukumu la kila Mkenya kuunga mkono juhudi hizo za kuhifadhi mazingira.

“Nyandarua ni kapu la chakula la taifa. Tuna ardhi bora na rutuba nzuri—tujivunie kaunti yetu na tuitumie kikamilifu. Chakula kinacholiwa nchini mzima kinatoka hapa. Tusikubali siasa za migawanyiko na kutengana; sisi ni watu wa kaunti maalum,” alisema Waziri Miano.

Kwa upande wake, PS Mbugua alitangaza ugawaji wa miche zaidi ya 5,000 ya miti na miti ya matunda kwa wakazi wa eneo hilo, kama sehemu ya juhudi za kitaifa za upandaji miti.

Aidha, aliwahimiza vijana wa Nyandarua kujisajili kwenye mpango wa NYOTA unaowalenga kwa mafunzo na ajira. Alifichua kuwa Nyandarua imetengewa nafasi 1,750, ambapo kila eneo bunge (Sub-County) litapata nafasi 70 kwa vijana.

“Hii ni nafasi ya kipekee kwa vijana wetu. Nawahimiza mjisajili na mtumie fursa hii kujikwamua kiuchumi,” alisema.

Lydia Mwangi
+ posts
Share This Article