Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa hapa Nchini imeonya uwezekano wa mafuriko na maporomoko ya ardhi, huku mvua inayonyesha katika maeneo kadhaa ikitarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya milimita 50.
Kwenye taarifa, idara hiyo imesema kiwango cha mvua kinachonyesha kote nchini kitaathiri takriban kaunti 30, ikiwemo Nairobi.
Ubashiri wa idara hiyo unaonyesha kuwa sehemu za eneo la ziwa Viktoria, Rift Valley, na nyanda za juu Magharibi mwa Rift Valley, itaongezeka na kuenea kwenye sehemu za Mashariki zikiwemo nyanda za juu Mashariki mwa Rift na nyanda za chini za kusini Mashariki kuanzia Alhamisi.
Idara hiyo ilionya kuwa mvua kubwa huenda ikanyesha kwenye baadhi ya maeneo ikiandamana na upepo mkali ambao huenda ukaharibu miti, nyaya za umeme na majengo hafifu.
Mvua hiyo kubwa pia inatarajiwa kuashiria mwanzo wa msimu wa mvua za masika wa mwezi Oktoba–Novemba–Disemba katika sehemu nyingi nchini.
