Kampuni nne za sukari zinazomilikiwa na serikali zimekodishwa kwa kampuni za kibinafsi, kwa kipindi cha miaka 30, katika kile wizara ya kilimo imesema ni kupiga jeki juhudi za kufufua sekta ya sukari hapa nchini.
Kulingana na waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, kampuni ya sukari ya nzoia sasa itasimamia na kampuni ya sukari ya West Kenya, ilhali kampuni ya sukari ya Chemilil sasa itasimamiwa na kampuni ya Kibos.
Kampuni ya miwa ya Sony imekodishwa kwa kampuni ya sukari ya Busia huku kampuni ya sukari ya Muhoroni ikiendeshwa na kampuni ya West Valley.
Aidha, Kagwe alisema kuwa wakati wa kipindi hicho cha ukodeshaji, hakuna ardhi ya umma ambayo itauzwa chini ya mkataba wa ukodeshaji.
Serikali imesema imeafikia makubaliano na chama cha wakulima wa miwa na washirika wake kulinda maslahi ya wafanyakazi wa viwanda vya miwa.
“Chini ya mkataba huo, serikali italipa madeni yanayodaiwa na wakulima na wafanyakazi wa kampuni hizo nne,” alisema Kagwe.
Wakati wa kipindi cha mpito cha miezi 12 kampuni hizo zitadadisi mahitaji ya wafanyakazi wa kampuni hizo kubaini mbinu ya kuwajumuisha kazini.
Serikali iliunda jopokazi la kutaadhmini changamoto za sekta ya sukari lililopendekeza mabadiliko kabambe ili kufufua uzalishaji sukari, kuimarisha usimamizi na kuboresha ushindani.