Maseneta wawasuta mawaziri kwa kukosa kufika bungeni kujibu maswali

Martin Mwanje
2 Min Read

Hamaki ilitanda katika Bunge la Seneti leo Jumatano asubuhi baada ya Waziri wa Utalii Rebecca Miano na mwenzake wa Afya Dkt. Deborah Barasa kukosa kufika bungeni.

Mawaziri hao walitarajiwa kuelezea utendakazi wa wizara zao na kujibu maswali ya Maseneta kuhusiana na masuala mbalimbali.

Hali hiyo ilisababisha Maseneta kupandwa mori na baadhi yao kutaka hoja ya kuwaadhibu iwekwe dhidi ya mawaziri wanaokosa kufika bungeni kueleza utendakazi wa wizara zao.

“Waziri Miano hakuwa mgonjwa lakini ameamua kwenda kuweka vifaru kengele katika hifadhi ya wanyama pori. Hiyo ni kusema ukinagalia katika taratibu ya venye wanambeba na uzito, anatuchukulia kwa urahisi kama bei ya chumvi. Ni kusema vifaru kwanza, Seneti ndio tunafuata,” alilalama Seneta wa kaunti ya Kirinyaga James Murango.

“Nafikiri imeibuka kuwa mazoea ya Mawaziri kutofika katika Bunge la Seneti. Nataka kuiomba Seneti kuanzisha hoja ya kuwaadhibu Waziri wa Utalii na Waziri wa Afya,” alipendekeza Seneta wa kaunti ya Marsabit Mohammed Chute.

“Asubuhi hii, nilipaswa kuwa nafanya kazi ya shule na mwanangu. Nililazimika kuiacha na kuja kuwasikiliza Mawaziri hawa. Sasa sijaweza kufanya kazi ya shule na mwanangu, na siwezi nikawauliza maswali,” alilalama Seneta wa kaunti ya Kitui Enoch Wambua.

“Kwangu mimi, hii ni asubuhi ambayo haijakuwa na tija. Bwana Spika, mambo yanapaswa kuanza kutendeka na yanapaswa kuanza kutendeka sasa hivi.”

“Rais amesema ni mpweke na hana mtu wa kumsaidia kupaza sauti ya kinachofanyika serikalini. Mawaziri wana fursa ya kupaza sauti yao juu ya kile ambacho serkali inafanya katika kuwahudumia Wakenya. Namtarajia Waziri wa Afya kuangazia suala la chanjo ya polio kwa watoto,” aliongeza Seneta mteule Esther Okenyuri.

Imekuwa ni mazoea kama ibada Maseneta kulalamikia hatua ya baadhi ya Mawaziri na nyakati zingine Magavana kukosa kufika katika Bunge la Seneti kujibu maswali.

 

Website |  + posts
Share This Article