Mahakama Kuu ya Kenya imetoa maagizo ya muda yanayomzuia MacDonald Mariga ambaye ni naibu rais wa shirikisho la soka la Kenya FKF kutekeleza majukumu ya kaimu Rais wa shirikisho hilo.
Katika uamuzi wake, mahakama imeelekeza kuwa hali iliyokuwepo kabla ya mabadiliko iendelee kubaki hadi kesi iliyowasilishwa na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa ya FKF itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Mahakama pia imeagiza pande zote zinazohusika katika mgogoro huo kuwasilisha majibu yao ndani ya muda uliowekwa kabla ya siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Kesi hiyo imepangwa kupangiwa maelekezo zaidi mwezi Mei 2026, ambapo hatua za mwisho za kisheria zitajadiliwa.
Uamuzi huu unakuja wakati kukiwa na mvutano wa uongozi ndani ya FKF na wadau wa soka wakisubiri mwelekeo wa mwisho wa mahakama kuhusu uhalali wa mabadiliko hayo ya uongozi.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kitaifa, NEC waliamua kumsimamisha kazi Rais wa FKF Hussein Mohamed na Mkurugenzi Mtendaji wa Kaimu Dennis Gicheru, wakiwatuhumu kwa ubadhirifu wa takriban shilingi milioni 42 za Mashindano ya Mataifa ya Afrika 2025, CHAN.
Kamati ilidai kuwa kulikuwa na utoaji wa zabuni bila ushindani na uwezekano wa wizi wa fedha, madai ambayo Hussein Mohamed alipinga mara moja akisema ni kinyume cha sheria na katiba, akidai hakupata nafasi ya kusikilizwa kwa haki na kwamba mkutano haukuitishwa ipasavyo.
Baraza la Migogoro ya Michezo liliingilia kati na kutoa amri za muda zilizozuia NEC kutekeleza kusimamishwa huko, hivyo kumrejesha Hussein Mohamed kwa muda.
Awali, NEC ilikuwa imemteua Naibu Rais FKF, McDonald Mariga kuchukua nafasi hiyo kwa muda, hatua ambayo ilisimamishwa na baraza hilo.