Rais wa Marekani, Donald Trump, Jumamosi alitishia kuharibu kabisa mitambo ya umeme ya Iran ikiwa Tehran haitafungua kikamilifu tena mlango wa bahari wa Hormuz ndani ya saa 48.
Tishio hili ni hatua kubwa ya kuongezeka kwa mvutano, siku moja tu baada ya Trump kuzungumzia kupunguza kasi ya vita.
“Iwapo Iran haitafungua KIKAMILIFU, BILA TISHIO, mlango wa bahari wa Hormuz ndani ya SAA 48 kuanzia wakati huu, Marekani itashambulia na kumaliza mitambo yao mbalimbali ya UMEME,” aliandika Trump.
Kiongozi huyo aliendelea kusema kwamba wataanza kwa kushambulia kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha nishati cha Iran kwenye chapisho lake katika mitandao ya kijamii.
Onyo la Trump huenda likaongeza wigo wa mashambulizi ya Marekani hadi miundombinu inayogusa maisha ya kila siku ya raia wa Iran.
Tishio la mashambulizi kutoka Iran limefanya meli nyingi zishindwe kupita katika mlango huo mwembamba wa bahari, ambao hutumika kama njia ya kupitisha takriban sehemu moja ya tano ya mafuta ya dunia na gesi asilia iliyoyeyushwa.
Hali hii inatishia kusababisha mshtuko wa nishati duniani ambapo, kukaribia kufungwa kwa mlango huo kulisababisha bei ya gesi barani ulaya kupanda kwa asilimia 35 wiki iliyopita.
Makao makuu ya jeshi la Iran yalisema Jumapili kwamba iwapo Marekani itashambulia miundombinu ya nishati ya Iran, Iran nayo italenga italenga miundombinu ya Marekani ya nishati, habari, teknolojia na mingine.