Kenya kuandaa kongamano la Afrika la afisi za bajeti bungeni

Marion Bosire
2 Min Read

Bunge la Kenya litaandaa awamu ya sita ya kongamano la mtandao wa Afrika wa afisi za bajeti bungeni baadaye mwezi huu jijini Mombasa.

Kongamano hilo ambalo litaandaliwa kwa ushirikiano kati ya mtandao wa Afrika wa afisi za bajeti bungeni – AN-PBO na afisi ya bajeti katika bunge la Kenya litaangazia ubadilishanaji mawazo kuhusu jinsi pesa zinaweza kutumiwa kutatua tatizo la maendelo barani Afrika na hali ya siku zijazo ya afisi za bajeti bungeni.

Kongamano hilo litafunguliwa rasmi na spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula na linatarajiwa kuhudhuriwa na wahusika kutoka Afrika na ulimwenguni kote wakiwemo wawakilishi wa afisi za bajeti za bunge na wa mashirika ya kimataifa ambayo husaidia mabunge katika kutathmini matumizi ya pesa za umma.

Mazungumzo hayo yataaangazia changamoto kadhaa zinazoukabili uchumi wa ulimwengu mzima wakati ambapo nchi zinajaribu kujijenga baada ya kukumbwa na janga la virusi vya korona.

Wadau wa kongamano hilo wataangazia pia migogoro iliyochipuza kutokana na vita vilivyoanzishwa na Urusi nchini Ukraine na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Kongamano hilo litajadili jinsi sera zinaweza kukabiliana na udhaifu wa kiuchumi unaoletwa na migogoro na jukumu la uangalizi katika kuhakikisha usimamizi bora wa fedha.

Jinsi ya kusimamia madeni ya umma hasa wakati ambapo hakuna uhakika ni suala ambalo pia litajadiliwa kwenye mkutano huo. Mazungumzo haya yanajiri wakati ambapo nchi zinashuhudia upungufu wa fedha kwa sababu ya janga la virusi vya korona na matukio mengine ya ukosefu wa utulivu.

Kongamano hilo litaandaliwa kati ya Agosti 27 na Septemba mosi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *