Marais wa Kenya,Uganda na Tanzania wakutana Zanzibar

Tom Mathinji
1 Min Read
Marais wa Kenya, Uganda na Tanzania wakutana Zanzibar.

Rais wa Kenya William Ruto, mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, wameshiriki mazungumzo visiwani Zanzibar, kujadili masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kupitia ukurasa wa X, Rais Ruto alisema wanakutana ili kuelezea kujitolea kwako kuimarisha utangamano na ustawi wa kanda hii.

Mkutano huo kati ya marais hao unaenda sambamba na mkutano wa Machi 14, 1996 wa Marais Daniel Arap Moi, Yoweri Museveni na Benjamin Mkapa ambao, uliweka msingi wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mawasiliano kutoka Ikulu nchini Tanzania imesema kuwa marais katika kikao hicho walikubaliana kuharakisha zoezi la ushirikishwaji wa wananchi kuhusu muundo na maeneo yatakayozingatiwa katika Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Zoezi hilo tayari limefanyika katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Kenya, Burundi na Uganda.

Inatekelezwa na timu ya wataalam inayojumuisha wajumbe watatu kutoka kila Nchi Mwanachama.

Shirikisho la Kisiasa, kulingana na Museveni, litahakikisha ustawi wa watu kupitia soko kubwa huku pia likihakikisha usalama wao wa kimkakati.

Shirikisho la Kisiasa litakapoundwa litajengwa katika mihimili mitatu; sera za pamoja za mambo ya nje na usalama, utawala bora na utekelezaji madhubuti.

Share This Article