Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini, KRA imesema ilikusanya shilingi trilioni 2.17 katika kipindi cha mwaka mmoja hadi Juni 30, 2023.
Hilo ni ongezeko la asilimia 6.7 ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.031 zilizokusanywa mwaka wa fedha uliotangulia.
Ingawa mapato yaliyotokana na ushuru yaliyokusanywa mwaka hadi mwaka yaliongezeka kwa shilingi bilioni 135, KRA bado haikufikia lengo la fedha zilizokusudiwa kukusanywa la shilingi trilioni 2.2.
Kaimu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo Rispah Simiyu anasema ukusanyaji ushuru uliathiriwa na uchumi wa nchi uliosinyaa hadi asilimia 4.8.
Anasema usinyaaji huo ulitokana na ukame wa muda mrefu ulioshuhudiwa mwaka jana na mzozo unaotokota kati ya Urusi na Ukraine na ambao unaendelea kutatiza mtungo wa usambazaji bidhaa.
“Mapato yaliyokusanywa yanaashiria kiwango cha asilimia 95.3 ikilinganishwa na fedha zilizolengwa. Huu ni mwaka wa pili mfululizo ambao KRA imezidi kiwango cha shilingi trilioni mbili,” aliongeza Simiyu.