Bingwa mara tatu wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio hizo Faith Kipyegon, atakutana kwa mara ya kwanza na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 10 Agnes Jebet Ng’etich, katika makala ya nne ya mashindano ya Absa Sirikwa Classic yatakayoandaliwa kesho eneo la Lobo Village, Kapseret, jijini Eldoret.
Akizungumza leo wakati wa kikao na wanahabari, Kipyegon, ambaye ni mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia ya mita 5,000, amesema atatumia mashindano ya kesho kufungua msimu, huku akilenga pia kushiriki mbio za mita 10,000 kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Agnes Jebet ambaye ni mshiriki wa mbio za nusu marathoni mwenye kasi zaidi amesema itakuwa fahari yake kuu kushindana na Kipyegn kwa mara ya kwanz akesho.
Wawili hao watashindana na Wakenya wenzao na wanariadha wengine wa kigeni akiwemo
Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Loice Chekwemoi wa Uganda, aliyeshinda makala ya pili ya mbio za nyika za Chepsaita.
Mshindi wa nishani ya shaba ya dunia mwaka 2023 katika mita 5000 Jacob Krop, atashiriki mbio za kilomita 10 wanaume ,akirejea kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2021.
Krop, atakutana na mshindi wa nishani ya fedha ya dunia mwaka 2022 katika mita 10,000 Stanley Mburu,mshindi wa zamani wa medali ya fedha ya dunia kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20 Leonard Bett, Keneth Kiprop, na Martin Kiprotich wote kutoka Uganda na Keny Kimutai wa Marekani.
Zaidi ya wanariadha 10,000 wanatarajiwa kushiriki mashindano ya kesho katika vitengo vya chipukizi chini ya umri wa miaka 20,kilomita 10 na kilomita 2 mzunguko mmoja kwa wanaume na wanawake.
Washindi wa kilomita 10 watatuzwa shilingi 780,000, washindi wa nishani za fedha 650,000, na watakaoshinda shaba wakituzwa shilingi 520,000.