Mahakama ya Kusuluhisha Migogoro ya Wafanyakazi imetoa agizo la kudumu la kuizuia Tume ya Taifa ya Polisi, NPSC, kujihusisha katika usajili wa maafisa wapya wa polisi.
Katika uamuzi wake leo Alhamisi, Jaji Hellen Wasilwa amesema tume hiyo haina mamlaka ya kuajiri, kutoa majukumu wala kuwatuma kazi maafisa wa polisi.
Jaji huyo ameongeza kuwa Inspekta Mkuu wa Polisi ana uhuru wa kuiamrisha Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, kufanya akitakacho.
Aidha, Jaji Wasilwa amelitaka bunge kurekebisha sheria mbili tata zinazozozaniwa ili kuepuka uingiliaji kati wa mamlaka ya Inspekta Mkuu wa Polisi.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na mbunge wa zamani wa Kilome, Harun Mwau.
NPS na NPSC zimekuwa zikilumbana mara kwa mara kuhusiana na utendakazi wake hili kila upande ukidai kuwa mamlaka kuliko mwingine.
Ni mivutano iliyosababishwa kuaihirishwa kwa zoezi la kuwasajili maafisa wapya 10,000 wa polisi lililokuwa limepangwa kufanyika kati ya Oktoba 3-9 mwaka huu.
Agizo la mahakama likiwa na maana kwamba Huduma ya Taifa ya Polisi iko huru kuanza tena mchakato wa kuajiri maafisa wapya wa polisi.