Mahakama Kuu yasimamisha fadhila za wakfu wa Bill & Melinda Gates

Marion Bosire
2 Min Read

Katika uamuzi uliotolewa leo Novemba 25, 2024, Mahakama Kuu imetoa maagizo ya muda ya kusitisha fadhila zilizokuwa zimetolewa awali kwa wakfu wa Bill & Melinda Gates.

Uamuzi huo unafuatia kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini, LSK kinachotaka mahakama isitishe fadhila hizo zilizotolewa kupitia kwa wizara ya masuala ya kigeni.

Jaji Bahati Mwamuye amesitisha kwa muda utekelezaji wa arifa ya kisheria iliyotolewa mapema mwaka huu hadi kesi iliyowasilishwa na LSK isikilizwe na kuamuliwa.

Vikao vya kusikiliza kesi hiyo vimepangiwa kuandaliwa mapema mwaka ujao wa 2025 huku kesi hiyo ikitajwa Februari 5, 2025.

Walalamishi wa kesi hiyo wameelekezwa kuwasilisha stakabadhi za kesi kwa washtakiwa kufikia mwisho wa siku ya tarehe 26 mwezi huu wa Novemba mwaka 2024 ambayo ni kesho.

Novemba 27, 2014, walalamishi watahitajika kusajili hati ya kiapo kuthibitisha mawasilisho hayo huku washtakiwa wakihitajika kuwasilisha majibu kufikia Disemba 10,2024.

Walalamishi watadurusu majibu na watakuwa na muda wa kutoa mawasilisho zaidi kutokana na majibu hayo kufikia Disemba 20, 2024.

Baada ya hapo walalamishi na wengine wanaotaka kujumuishwa kwenye kesi hiyo watatoa mawasilisho ya maandisho ya kesi hiyo kufikia mwisho wa Januari 8, 2025.

Washtakiwa wanatarajiwa kutoa mawasilisho yaliyoandikwa ya kujibu walalamishi kufikia mwisho wa siku ya Januari 22, 2025.

Website |  + posts
Share This Article