Waziri Kagwe ataka ufadhili wa sekta ya kilimo kuongezwa

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe.

Waziri wa kilimo Mutahi Kagwe ametoa wito kwa umma kutoa maoni kuhusu ufadhili wa kilimo kupitia kwa bajeti ya kitaifa.

Akiongea wakati wa mkutano  wa mwaka huu kuhusu ufadhili wa kilimo cha mazao ya chakula (FINAS) , Kagwe alishangaa ni kwa nini sekta ya kilimo inapokea asilimia tatu pekee ya mgao kwenye bajeti ya kitaifa  licha ya kuchangia asilimia hamsini kwenye pato la jumla la kitaifa.

Hata hivyo alisema ipo mipango ya kushauriana na hazina kuu, bunge na watunga sera wengine ili kuongeza mgao wa bajeti ya sekta ya kilimo.

Kagwe aliongeza kusema kuongezwa kwa bajeti hiyo kutaileta Kenya kwenye nafasi nzuri ya kutekeleza azimio la Malabo la mwaka 2024 na azimio la kampala la mwezi Januari mwaka huu na  vile vile kuleta mabadiliko katika  sekta hiyo kama vile kuongeza uzalishaji wa kilimo kwa asilimia 45, kukomesha hasara ya mavuno na kuimarisha biashara ya mazao ya kilimo kati ya mataifa ya Afrika.

Wakati huo huo, waziri Kagwe alitoa wito kwa benki kutimiza mahitaji ya wakulima akisema kwa wakati huu asilimia tatu pekee ya mikopo ya dola billioni 49 iliyotolewa na benki mwaka 2023 ilielekezwa kwa sekta ya kilimo.

Matamshi hayo yaliungwa  mkono na makamu wa rais wa mpango wa utoaji huduma wa AGGRA, Hamadi Boga.

Website |  + posts
Share This Article