Maaskofu wa Kanisa Katoliki wametoa wito kwa Rais William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odiinga kulegeza misimamo yao mikali na kushiriki meza ya mazungumzo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini Martin Kivuva, maaskofu hao waaidha wameutaka muungano wa upinzani wa Azimio kutafuta njia mbadala ya kushinikiza malalamiko yao badala ya maandamano ambayo yamesababisha vifo na uharibifu wa mali siku zilizopita.
“Muungano wa Azimio unapaswa kutafuta njia mbadala ambayo haitailemeza nchi, kusababisha vifo, vurugu na uharibifu wa mali,” alisema Askofu Kivuva wakati akiwahutubia kikao cha wanahabari katika mtaa wa Karen leo Jumatano.
Maaskofu hao pia walitoa wito wa kufufuliwa kwa mazungumzo kati ya serikali ya Kenya Kwanza na Azimio ili kuangazia masuala yanayoibuliwa na upinzani.
Hata hivyo, kinyume cha awali ambapo mazungumzo hayo yalijumuisha wanasiasa kutoka upande wa serikali na upinzani, maaskofu hao wanataka viongozi wa kidini, taasisi na watu wengine mashuhuri kujumuishwa kwenye mazungumzo hayo ili kuhakikisha ufanisi wake.
Kuhusiana na suala la gharama ya maisha, walitoa wito kwa Rais William Ruto kubatilisha sheria ya fedha ya mwaka 2023 waliyosema imefanya hali ya maisha kuwa ngumu zaidi kwa Wakenya wengi wa tabaka la chini.
“Rais Ruto anapaswa kubatilisha sheria ya fedha ya mwaka 2023 na kutafuta njia mbadala itakayohakikisha maalengo sawia yanaafikiwa bila kusababisha mzigo wa maisha kuwaelemea Wakenya,” alisema Askofu Anthony Muheria wakati wa kikao hicho.
Wito wa maaskofu hao unakuja wakati muungano wa Azimio umeapa kufanya maandamano ya siku tatu kuanzia leo Jumatano hadi Ijumaa.
Serikali kwa upande mwingine imeapa kuhakikisha hakuna maandamano yatakayofanyika katika kipindi hicho na maafisa wa usalama kwa sasa wanashika doria katika sehemu mbalimbali za nchi ili kuhakikisha shughuli zinaendelea kama kawaida.