Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema serikali haitakubali upinzani kufanya maandamano yoyote ya vurugu nchini akiongeza kuwa uharibifu wa mali ni jambo lisiloweza kuruhusiwa.
Gachagua alisema maandamano ya hivi maajuzi yalikuwa ya vurugu na yaliyokumbwa na visa vya wazi vya uporaji kiasi kwamba hayawezi kukubaliwa siku zijazo.
Aliyasema hayo leo Ijumaa wakati wa mazishi ya mpiganiaji wa Mau Mau John Njigoya Kagwe ambaye pia alijulikana kama Brigadia Kiboko yaliyofanyika katiks shule ya upili ya Ngorika katika eneo la Ol Kalou, kaunti ya Nyandarua.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga.
Gachagua akitumia fursa hiyo kusema mbele ya Raila aliyeitisha maandamano ya upinzani kwamba ingawa katiba inaruhusu maandamano ya amani, hairuhusu uharibifu wa mali ya watu na uporaji.
“Katiba yetu ina vifungu vinavyoruhusu kufanyika kwa maandamano, hiyo ndio sababu tuliruhusu kufanyika kwa maandamano. Lakini kile mlichokifanya tu ni kuharibu mali ya watu na kuwaibia Wakenya na kupigana na polisi. Maandamano yalihusu tu wizi na uporaji. Hiyo haiwezi ikakubaliwa kamwe humu nchini. Hatutakubali yafanyike tena nchini,” alisema Gachagua.
Kadhalika Naibu Rais aligusia mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali na upinzani akisema hakuna ubaya yakifanyika ila hawatakubali serikali ya muungano na mazungumzo ya kugawana serikali.
“Mazungumzo yanaweza yakaendelea. Tumemtuma kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah na mumemtuma Kalonzo Musyoka. Timu hizo zinaweza zikazungumza. Lakini hakuna siku ambayo tutaruhusu uharibifu wa mali kwa kisingizo cha kufanya maandamano. Hakutakuwa na serikali ya muungano,” aliongeza Gachagua.
Kwa mujibu wa Naibu wa Rais, shabaha yao itakuwa kukuza maendeleo nchini na kuboresha maisha ya Wakenya kupitia mipango ya maendeleo inayoendelea.