Balozi wa China humu nchini Zhou Pingjian siku ya Jumatatu alimtembelea Rais mstaafu Uhuru Kenyatta afisini mwake jijini Nairobi.
Taarifa kutoka kwa afisi ya Rais huyo mstaafu, ilisema kuwa Uhuru alitambua ushirikiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizi mbili na jinsi ulivyochangia pakubwa katika utekelezaji wa maendeleo wakati wa uongozi wake wa nchi hii.
Ziara hiyo imewadia huku nchi hizi mbili zinapojiandaa kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano kati ya Kenya na China.
Balozi Zhou alikariri kwamba uhusiano huo umekuza ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kitamaduni kati ya nchi hizi mbili.
Uhuru naye alimuarifu balozi huyo wa China kuhusu jukumu lake jipya barani Afrika la kutafuta amani na usalama.
Alisisitiza kwamba amani ndio msingi wa maendeleo na kwamba Afrika inaweza tu kufikia malengo yake endapo amani itadumishwa katika mataifa yote ya Afrika.
Maadhimisho hayo yataandaliwa Alhamisi ijayo katika ofisi ya biashara duniani iliyo Westlands jijini Nairobi.
Siku chache zilizopita, balozi wa Marekani humu nchini Meg Whitman na mwenzake wa Uingereza Neil Wigan pia walimtembelea Uhuru ofisini mwake jijini Nairobi.