Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC leo Jumanne imewakamata maafisa wanne waandamizi wa kuanti ya Taita Taveta kwa tuhuma za kufuja fedha za umma zenye thamani ya shilingi milioni saba.
Maafisa hao ni Thomas Jumwa ambaye ni mshauri wa sasa wa masuala ya kiuchumi wa Gavana wa kaunti hiyo, Liverson Mghendi ambaye ni Katibu wa zamani wa kaunti hiyo na Leonard Langat ambaye ni Afisa Mkuu wa zamani wa Fedha. Wote hao walikamatwa ndani ya kaunti ya Taita Taveta.
Mshukiwa wa nne, Christine Wakera ambaye ni Afisa Mkuu wa zamani wa Biashara, Utalii na Ustawi wa Vyama vya Ushirika alikamatwa mjini Eldoret.
Kwenye taarifa, Msemaji wa EACC Eric Ngumbi amesema washukiwa hao walikamatwa kwa tuhuma za kufuja shilingi hizo milioni saba kwa kusingizia kuwa wanafanya maadhimisho ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia kati ya Novemba 24 na 27, 2022.
Washukiwa hao wanne kwa sasa wanapelekwa katika ofisi za EACC za kanda ya Pwani mjini Mombasa ili kuandikisha taarifa.
Kisha watazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mombasa Central wakisubiri kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kupambana na Ufisadi, EACC Oktoba 23, 2024.