Kwale yaongeza ada ya kuingiza muguka

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani ametangaza kuongezwa kwa ada ya kuingiza muguka katika kaunti hiyo. Ada hiyo imekuwa shilingi elfu 10 kwa kila lori na sasa imepandishwa hadi elfu 300.

Lengo la hatua hiyo, kulingana na Achani, ni kuzidisha bei ya zao hilo na hivyo kuwavunja moyo wakazi wa kaunti ya Kwale wanaolitumia.

Aliendelea kufafanua kwamba hatua hiyo imeratibishwa na mswada wa kifedha wa kaunti uliopitishwa katika bunge la kaunti ya Kwale na ambao unasubiri saini yake ili kuanza kutekelezwa.

Achani ameshangaza wengi na hatua hii hasa baada ya kukosa kupiga marufuku zao la muguka kama wenzake wa Mombasa na Kilifi lakini marufuku hiyo ilibatilishwa.

Viongozi wa eneo la Pwani wanapinga mauzo na matumizi ya muguka katika himaya zao kwa kile wanachokitaja kuwa athari zake mbaya hasa kati ya vijana.

Muguka ni mmea halali nchini na mauzo na matumizi yanakubalika kulingana na sheria ya mimea ya mwaka 2013 na kanuni za Miraa zilizopitishwa na bunge la kitaifa mwaka 2023.

Gavana Abdulswamad Nassir ndiye alikuwa wa kwanza kutangaza marufuku ya muguka, akafuatiwa na mwenzake wa Kilifi Gideon Mung’aro na Andrew Mwadime wa Taita Taveta akawa wa tatu.

Hata hivyo, mahakama kuu ya Embu ilisitisha utekelezaji wa marufuku hiyo hadi kesi ya kuipinga itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Share This Article