KUPPET yatakiwa kufutilia mbali mgomo wa walimu

Martin Mwanje
1 Min Read
Mgomo wa walimu wa KUPPET wasimamiswa na mahakama.

Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo, KUPPET kimetakiwa kufutilia mbali mgomo wa walimu wa shule za sekondari ulioanza leo Jumatatu kote nchini. 

Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema haoni haja ya malumbano wakati serikali tayari imeelezea kujitolea kwake kuangazia masuala yaliyoibuliwa na walimu.

“Kwa hivyo, natoa wito wa KUPPET kutafakari upya msimamo wao na kufutilia mbali mgomo. Serikali imeonyesha utayari wake wa kuangazia masuala yaliyoibuliwa. Kwa hivyo hatuoni sababu ya malumbano,” alisema Waziri Ogamba katika taarifa.

Alitoa mfano wa shilingi bilioni 21.8 ambazo tayari zimetolewa na serikali kwa shule za msingi, JSS na shule za sekondari.

“Sasa tunatarajia kwamba shule zitarejelea shughuli zao vizuri na masomo yataendelea bila matatizo yoyote.”

Waziri Ogamba aliyasema hayo baada ya kutembelea shule kadhaa za msingi na JSS katika kaunti za Machakos, Kajiado na Nairobi leo Jumatatu.

Ripoti zinaashiria kuwa shule za msingi zilifunguliwa leo Jumatatu kote nchini kama ilivyopangwa baada ya chama cha KNUT kufutilia mbali mgomo uliokuwa umeitishwa kushinikiza kutekelezwa kwa mkataba wa walimu wa mwaka 2021-2025.

KNUT imesema ilichukua hatua hiyo baada ya kuona kusudi la serikali la kuangazia matakwa yao.

 

Share This Article