Siku chache baada ya wanaharakati wa Kenya kuzuiwa kuingia Tanzania, na kushuhudiwa kwa cheche za maneno kati ya baadhi ya raia wa nchi hizo mbili, Rais William Ruto leo Jumatano ameomba msamaha nchi jirani ya Tanzania na Uganda.
Akizungumza wakati wa maombi ya kitaifa katika hoteli ya Safari Park jijini Nairobi, kiongozi wa taifa alisema nchi hii kwa sasa imechukua mkondo wa maridhiano kwa kuzingatia maudhui ya mwaka huu ya maombi hayo “Inuka na Ujenge Upya”.
“Majirani wetu kutoka Tanzania, ikiwa tumewakosea kwa njia yoyote, tusamehe. Marafiki wetu kutoka Uganda, ikiwa kuna jambo Kenya imefanya ambalo sio sahihi, tunaomba msamaha,” alidokeza Rais Ruto.
Rais alisema juhudi za kujenga upya taifa hili zinazaa matunda, akisema uchumi wa taifa hili unaimarika huku miradi na mipango ya serikali ikiendelea kuboresha maisha ya Wakenya.
“Tunapaswa kushirikiana katika jitihada za kuhakikisha usawa wa kila mmoja, Ujumuishaji na Ufanisi,” aliongeza kiongozi wa Taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki alisema taifa hili lina fursa ya kujenga upya uhusiano kama wananchi, majirani na kati ya vizazi licha ya changamoto zilizopo.
“Taifa linaloomba pamoja, huishi pamoja,” alisema Prof. Kindiki.
Maombi hayo yalihudhuriwa na Wabunge, Mawaziri na Maafisa Wakuu serikalini miongoni mwa wengine.