Kundi la Nihon Hidankyo la Japani lashinda Tuzo ya Amani ya Nobel

Martin Mwanje
2 Min Read

Kundi la manusura wa bomu la atomiki la Japani la Nihon Hidankyo limeshinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu. 

Kundi hilo linalopinga matumizi ya silaha za nyuklia limetunukiwa tuzo hiyo leo Ijumaa.

Kundi hilo la mashinani linajumuisha manusura wa bomu la atomiki katika miji ya Hiroshima na Nagasaki.

Manusura hao hufahamika mno kama Hibakusha.

Kundi hilo liliasisiwa mnamo mwaka wa 1956.

Lilitunukiwa tuzo hiyo “kutokana na juhudi zake za kufikia dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia na kwa kudhihirisha kupitia shuhuda za mashahidi kwamba silaha za nyuklia kamwe hazipaswi kutumika tena,” alisema Jorgen Watne Frydnes, mwenyekiti wa Kamati ya Nobel ya Norway mjini Oslo.

Kamati hiyo ilielezea tahadhari kuwa “mwiko wa nyuklia” wa kimataifa uliojiendeleza kufuatia mashambulizi ya bomu la atomiki ya Agosti, 1945 “upo chini ya shinikizo”.

“Tuzo ya mwaka huu ni tuzo inayotilia mkazo umuhimu wa mwiko huu wa nyuklia. Na sote tuna wajibu, hasa nchi zenye nguvu za nyuklia,” Frydnes aliwaambia wanahabari wakati wa hafla ya kumtangaza mshindi wa tuzo hiyo.

Mwaka jana, mshindi wa tuzo hiyo alikuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu aliyefungwa jela Narges Mohammadi.

Mohammadi alitunukiwa tuzo hiyo kwa kupambana na ukandamizaji wa wanawake nchini Iran.

Tuzo hiyo hutolewa pamoja na medali ya dhahabu, stashahada na tuzo ya dola milioni moja.

Tuzo hiyo itatolewa wakati wa hafla rasmi itakayoandaliwa mjini Oslo Disemba 10 mwaka huu.

 

Share This Article