Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC limefurika watu wengi ambao waliamka asubuhi na mapema kushuhudia kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Prof. Kithure kindiki.
Viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Makatibu, Wabunge, Maseneta, Magavana na wakuu wa mashirika mbalimbali ya serikali tayari wameketi na kutulia tuli wakisubiri kushuhudia hafla hiyo.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor wameonekana wakiwa wenye shughuli nyingi kuhakikisha mambo yanakwenda sawa wakati wa uapisho huo.
Prof. Kindiki tayari amewasili katika eneo la KICC.
Kuapishwa kwake kuwa Naibu Rais kunafuatia hatua ya mahakama kuondoa maagizo yaliyomzuia kula kiapo tangu alipoteuliwa kwenye wadhifa huo na Rais William Ruto.
Hii ilifuatia hatua ya mtangulizi wake Rigathi Gachagua kupinga kuapishwa kwake kwa madai kuwa hakuondolewa kwenye wadhifa huo kwa mujibu wa katiba.
Usalama umeimarishwa maradufu wakati taifa likifuatilia hafla hiyo kwa karibu ikizingatiwa leo Ijumaa imetangazwa sikukuu.