Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR inasema hadi kufikia sasa, imebaini kuwa jumla ya watu 39 walifariki wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 yaliyofanywa wiki jana.
Inasema miili mingi ya waathiriwa bado haijafanyiwa upasuaji kubaini kiini cha vifo hivyo.
Watu wengine 361 walijeruhiwa katika maeneo mbalimbali kote nchini, kwa mujibu wa data zilizokusanywa na tume hiyo kati ya Juni 18 na Julai 1, 2024.
Kulingana na KNCHR, watu 17 wameripotiwa kufariki Nairobi, Nakuru (3), Laikipia (1), Narok (1), Kajiado (3), Uasin Gishu (4), Kakamega (1), Kisumu (2) na Kisii (1).
Wengine waliofariki ni Mombasa (3), Siaya (1), Kiambu (1) na Nandi (1).
“Tume inaendelea kulaani vikali matumizi yasiyotakikana ya vurugu na mabavu ambayo yalitumiwa dhidi ya waandamanaji, matabibu, wanasheria na wanahabari, na katika maeneo salama kama vile kanisani, vituo vya dharura vya utoaji tiba na ambulensi,” alisema Roseline Odede, mwenyekiti wa KNCHR katika taarifa.
Odede kadhalika amelaani uharibifu wa miundombinu mbalimbali uliofanywa na baadhi ya waandamanaji hao.