Nyadhifa zote zilizo wazi za Machifu na Manaibu wao zitajazwa ndani ya siku 90 zikihusisha zile ambazo mchakato wa kuwahoji watu wa kuzijaza tayari umekamilika.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki anasema kuna mipango ya kuwaajiri na kuwapeleka Machifu na Manaibu wao kujaza nyadhifa zilizo wazi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Nyadhifa hizo zilisalia wazi kutokana na vifo, kufutwa kazi kwa maafisa baada ya kesi zao kukamilika mahakamani au kushughulikiwa na Tume ya Utumishi wa Umma na hakuna rufaa iliyowasilishwa mahakamani, kupandishwa vyeo kwa maafisa waliohudumu katika nyadhifa hizo, kujiuzulu au maafisa kukabidhiwa majukumu mapya,” alisema Waziri Kindiki alipokuwa akihojiwa katika bunge la Seneti leo Jumatano.
Kuna jumla ya kata 3,955 na kata ndogo 9,045 kote nchini zinazohudumiwa na Machifu na Manaibu wao, na serikali inalenga kujaza nyadhifaa zilizosalia wazi katika hatua inayolenga kuimarisha usalama kila pembe ya nchi.