Kenya imekabidhiwa jukumu la kuongoza harakati za kukomesha biashara ya silaha ndogo ndogo katika eneo la maziwa makuu na upembe wa Afrika.
Kenya inachukua uenyekiti wa kituo cha kanda kuhusu silaha ndogo ndogo, RECSA kufuatia uamuzi wa pamoja wa wawakilishi wa nchi 15 wanachama.
Katibu katika Wizara ya Mambo ya Ndani Dr. Raymond Omollo, alisema jukumu hilo linapanua wajibu wa Kenya katika juhudi za kukomesha biashara hiyo na kuendeleza ulinzi na amani ya kudumu katika kanda.
Akizungumza kwenye mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama mjini Kinshasa, DRC, Omollo alisema kwamba Kenya imejitolea kuunga mkono juhudi dhidi ya silaha ndogo kwa shari kubwa.
Alielezea utayari wa Kenya kuendeleza ajenda ya RECSA ambayo inajumuisha kumaliza mizozo, ugaidi, uhalifu na migogoro ya kibinadamu ambayo inasababishwa na kuendelezwa na silaha ndogo ndogo.
“Tutatumia mbinu jumuishi ambayo itahusisha mpango wa kupokonya watu silaha, kukomesha uwezo wa wahalifu kwenye makabiliano na kuihamasisha tena na jamii. Tunakusudia kuimarisha ushirikiano, mashirika ya kikanda na washirika wa kimataifa kupiga jeki juhudi za kupeana habari na kufahamu, kuzuia na kuwajibikia biashara hiyo haramu,” alisema katibu Omollo.
Kenya imekuwa ikihudumu katika wadhifa wa naibu mwenyeketi huku DRC ikiwa mwenyekiti katika baraza hilo la mawaziri, chombo kikuu cha kutoa mwelekeo katika kituo cha RECSA.
Baraza hilo linajumuisha Mawaziri wa Mambo ya Ndani katika nchi wanachama.
Kati ya majukumu ya kwanza ya Kenya ni kuimarisha ushawishi wa RECSA katika bara zima la Afrika katika maswala ya usalama na amani.
Kenya imetakiwa iwasilishe ombi kwa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika kutambua RESCA kama mojawapo ya mashirika yake ambalo litahusika na maswala ya silaha ndogo ndogo.