Kenya yasema ushuru mpya wa Marekani ni fursa nzuri ya kujiendeleza

Martin Mwanje
2 Min Read
Lee Kinyanjui - Waziri wa Biashara

Kenya imesitisha kimya chake kuhusiana na awamu mpya ya ushuru mkubwa wa forodha uliotangazwa na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump jana Jumatano.

Akitangaza ushuru huo, Trump alisema ushuru wa kiwango cha chini wa asilimia 10 utawekwa kwenye bidhaa zinazoingia kutoka nchi zote kuanzia Jumamosi hii.

Ameonya kuwa ushuru wa forodha wa kutendeana utakaonza kutekelezwa tarehe 9 mwezi huu utakuwa wa kiwango cha juu hata zaidi.

Akizungumzia kutangazwa kwa ushuru huo, Waziri wa Biashara wa Kenya Lee Kinyanjui amesema ushuru huo utaibua changamoto si haba kwa nchi hiyo lakini pia fursa lukuki.

“Ingawa bidhaa za Kenya zinazouzwa nchini Marekani sasa zitatozwa ushuru wa forodha wa asilimia 10, hiki ni kiwango kidogo zaidi kuliko viwango vilivyowekwa kwa washindani wakuu wa kutengeneza nguo kama vile Vietnam (46%), Sri Lanka (44%), Bangladesh (37%), China (34%), Pakistan (29%) na India (26%,” alisema Kinyanjui kwenye taarifa.

Kulingana na Waziri huyo, fursa zinazojitokeza kwa Kenya kutokana na uwekaji wa ushuru huo ni pamoja na kuwa kinara katika utengenezaji wa nguo,  uwezo mpya wa kutengeneza bidhaa na serikali kuunga mkono ukuaji wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi,

Kinyanjui ametaja changamoto kuu ambayo Kenya itakumbana nayo kutokana na kutangazwa kwa ushuru huo mpya wa Marekani kuwa gharama zilizoongezeka za bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Trump alitangaza kuwekwa kwa ushuru mkubwa wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi zote duniani wakati wa tukio lililoandaliwa katika Ikulu ya Marekani jana Jumatano.

Kwa mujibu wa tangazo lake, China imewekewa ushuru wa forodha wa asilimia 34 , India (26%) huku kiwango cha ushuru kwenye bidhaa kutoka Umoja wa Ulaya (EU)  kikiwa asilimia 20.

 

Website |  + posts
Share This Article